Ibada Tarehe 14/8/2022, SOMO : UONGOZI

 Mchungaji ,

VICTOR GASPER MALAMLA

+ Yohana 14:16-18, "Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele;.." Kabla ya kuanza jambo lolote hakikisha unakaribisha uwepo wa Roho Mtakatifu. Kuna sauti ya Mungu baba, Mungu mwana na Mungu Roho Mtakatifu, Wote wanaongea ila anaeweza kutafsiri ni Roho Mtakatifu. Ukishaokoka anaekaa ndani yako ni Roho Mtakatifu na yeye ndiye anayetukumbusha kwa habari ya toba na rehema pale tunapokosea. Roho Mtakatifu ndiye msaidizi na kiongozi wetu, bila yeye hatuwezi kufika popote.
 
+ 1 Timotheo 3:1 -Ni neno la kuaminiwa;  mtu akitaka kazi ya askofu, atamani kazi njema..."
Uongozi unaanzia nyumbani, Mtoto inabidi umlee katika malezi ambayo hata akikua atakukumbuka kwa kumfanya kiongozi bora. Hata kama umesoma sana kama haujasoma uongozi ni ngumu sana kufikia malengo yako na ubaadae wako. Kila aliyeumbwa na Mungu anachembechembe za uongozi ndani yake. Kazi yetu ni kuichochea ile mbegu ili itoe matunda mazuri. Hauwezi kuwa kiongozi bora kwa kusoma biblia tu, ndio maana kuna semina na madarasa mbalimbali.
 
- Unavyotaka kuwa kiongozi ni lazima ujifunze zaidi kuhusu kuongoza watu na fedha. Fedha inaongozwa kwa hekima sio kwa kudunduliza. Ukitaka kufanikiwa weka kiwango cha maisha yako na usizidishe hapo iwe na nidhamu katika mipango yako. Usilazimishe kuishi viwango ambavyo haujafika. Hakikisha unaongeza kiwango chako cha uongozi. Kiongozi ni mtu yeyote anaeweza kuhakikisha mwingine anakamilisha majukumu yake kupitia yeye.
 
-Kiongozi ni yule anayetimiza majukumu yake, hauna haja ya kukaa na kuanza kujitambulisha ukifanya vyema kila mmoja atakutambua. Usipokuwa na hekima na ufahamu juu ya uongozi Mungu hawezi kukutumia kwa mambo makubwa. Mungu anatafuta watenda kazi, watenda kazi sio manabii, mitume, wainjilisti na wachungaji tu. Wafanya biashara na wanaomiliki fedha pia ni watenda kazi kwa sababu wanasababisha kazi ya Mungu isonge mbele na kuujenga ufalme wa Mungu.
 
-Tutamiliki, kutawala na kuvuka mipaka tukiongeza maarifa. Hauwezi kuongoza biashara yako ikafanikiwa kama sio mwaminifu katika kulipa zaka. Ukitaka mafanikio ya haraka kupotea ni rahisi mno, hakikisha unafuata itifaki zote. Ukitaka kuwa kiongozi lazima uwe na bidii, ufahamu, maarifa na hekima ya Mungu ndani yako.
 
MAJUKUMU YA KIONGOZI

-Yakupasa kuwa sababu ya kupunguza kelele au kuziondoa kabisa mahali ulipo.
- Lazima uonyeshe tabia unayoendana na nafasi yako. Kwa sababu kiongozi ni mtu anayetaazamwa na watu wengi. Fanya kile unachotamani wale unaongoza wakifanye.
- Lazima awe mfano kwenye kutenda haki na sio udhalimu, fanya mambo bila kupendelea yeyote.
- Usikubali kuongoza watu kwa maneno ya kusikia, mashauri ya wengi sio mashauri ya Mungu. Kiongozi lazima uwe na Roho anaekusaidia kupambanua.
- Kunyesha uadilifu na tabia njema sawasawa na nafasi yako.
-Ni kazi yako kugawa majukumu na madaraka kwa wengine ili usionekane ni mungu mtu, kwamba bila wewe mambo mengine hayaendi.
 
ANGUKO LA UONGOZI

- Ukiona kiongozi anaanza kumilikiwa na kiburi, hawezi kufika mbali. Kiburi ni ile hali unaelekezwa na kuambiwa jambo lakini hautekelezi. Kiburi kinaambatana na roho ya ujuaji, hataki kuelekezwa kwa chochote anajifanya anajua kila kitu. Elimu na kipawa husababisha kiburi kwa watu wengi. Ni vizuri uwe makini ili ufikie mwisho ulio mwema.
- Ukiona unapenda fedha na mali kuliko utu. Utajuaje mtu anapenda mali na fedha ni kwamba hayupo
- Hasira, hakikisha hauongei wala kujibu chochote ukiwa na hasira. Maana unaweza kutoa majibu yasiyopendeza yakakufanya udharaulike katika nafasi yako.
- Uzinzi na uasherati utakufanya ujitenge mbali na uwepo wa Mungu, hivyo kuanguka ni lazima.
- Kushindwa kuvumilia, katika uongozi unaweza kukutana na mabaya mengi ni kumuomba Mungu akupe neema ya kushinda na kuhimili mabaya. Haijalishi watu wameongea mabaya kiasi gani kwako nyamaza kimya kwa kadri unavyoendelea kuongea unafanya mambo yazidi kuwa mengi. Kuna baraka nyingi katika kunyamaza.
 
+Mathayo 5:11-12, "Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu..."


Comments

Popular posts from this blog

Ibada tarehe : 21/8/2021 Somo : UHARIBIFU

IBADA YA JUMAPILI TAREHE 28.08.2022, SOMO : ROHO YA UCHAWI